Jumapili , 6th Oct , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemwagiza kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Singida kuwachunguza watumishi 48 wa Halmashauri ya Iramba kwa tuhuma za upotevu wa fedha.

Waziri Mkuu alipokuwa Ndago Iramba

Ametoa agizo hilo leo Jumapili, Oktoba 6, 2019, wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ndago mara baada ya kukagua majengo ya kituo cha Afya, na kueleza kuwa hajaridhishwa na ujenzi wa kituo cha afya cha Ndago, wilayani Iramba mkoani Singida kwa sababu uko chini ya kiwango.

“Nimepita kote nchini kukagua vituo hivi lakini hapa wamenikasirisha. Wamenileta kwenye jengo nilikaguem nikajua ni jipya kumbe ni la zamani. Lazima nikiri kwamba fedha yetu hapa haijakamilika, jengo la mama na mtoto halijakamilika. Nilipouliza linakamilika lini, wananijibu tuko kwenye final touches (tuko hatua za mwisho),” amesema.

Alipomuuliza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw, Leno Mwageni amebakiza kiasi gani cha fedha katika sh. milioni 400 ambazo zililetwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo, Mkurugenzi huyo alijibu kwamba hakuna kiasi cha fedha kilichobakia.

“Jengo lile halivutii kabisa, wanaotoa maelezo hakuna kinachoeleweka. Sijaridhishwa kabisa na hali hii. Jengo la upasuaji nalo pia nimeona ni la zamani. Hii ina maana hamjajenga jengo jipya. Mimi nataka nione jengo jipya hapa,” amesisitiza.

Zaidi Tazama Video hapo chini