Jumatano , 10th Mei , 2023

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Imarn Khan amekamatwa mapema mjini Islamabad muda mfupi baada ya kutoka mahakamani alikofikishwa kusikiliza kesi yenye mashtaka chungunzima ya rushwa na ufisadi.

Kulingana na taarifa za mashirika mawili ya habari lile la Associated Press na AFP, Khan alikamatwa nje ya mahakama kwenye Mji Mkuu wa Pakistan, Islamabad na maafisa wa taasisi ya kushughulikia uwajibikaji wa viongozi wa umma.

Saa chache baada ya kusambaa taarifa za kukamatwa kwake mamia ya wafuasi wake waliteremka mitaani kwenye miji kadhaa ya Pakistan kulaani kisa hicho. Polisi ilipambana na wafuasi wa Khan kwa kutumia maji ya kuwasha na mabomu ya machozi kwenye miji ya Karachi, Lahore, Islamabad, Rawalpindi na Peshawar.

Mawakili na mashuhuda wamesema maafisa hao walimvizia kiongozi huyo, wakamkamata kwa nguvu, wakamshambulia na kisha wakamburura hadi kwenye gari yao na kuondoka naye kusikojulikana.

Aquil Niazi ni mmoja ya mawakili wa Khan "Leo (Khan) alipokwenda kuchukuliwa alama za vidole, walimkamata kwenye viunga vya mahakama. Wakampiga kwa fimbo kichwani halafu wakampulizia kitu ambacho nusra kimfanye apoteze fahamu. Nadhani walimpulizia kitu. Baadaye wakamwingiza kwenye gari"