Jumamosi , 6th Sep , 2025

"Yeye (Putin) anaweza kuja Kyiv...siwezi kwenda Moscow wakati nchi yangu inapigwa makombora, inashambuliwa kila siku. Siwezi kwenda kwenye mji mkuu wa gaidi huyu" amesema Zelensky.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemtaka Vladimir Putin kwenda Kyiv kwa mazungumzo ya kumaliza vita alivyoanzisha, baada ya kukataa ofa ya kiongozi huyo wa Urusi ya kwenda Moscow.

Hata hivyo Putin amesema hatasafiri popote kwa mazungumzo na mwenzake wa Ukraine, na amependekeza kuwa atakuwa tayari kufanya mkutano huko Moscow.

Katika mahojiano na shirika la habari la ABC News, rais wa Ukraine amepuuzilia mbali uwezekano wa kwenda Moscow, Urusi, akisema hawezi kwenda mji mkuu wa “gaidi huyo."

"Yeye (Putin) anaweza kuja Kyiv...siwezi kwenda Moscow wakati nchi yangu inapigwa makombora, inashambuliwa kila siku. Siwezi kwenda kwenye mji mkuu wa gaidi huyu."

Yuriy Boyechko, Mkurugenzi Mtendaji wa Hope for Ukraine, ambayo inaunga mkono jamii zilizo mstari wa mbele wa vita, ameiambia Newsweek kwamba mwaliko wa Putin ulikuwa ni hatua ya kimkakati ya kumdanganya Rais Trump wa Marekani, ambaye anashinikiza viongozi hao kukutana.

Maoni ya Zelensky yanakuja wakati matarajio ya mazungumzo na Putin kumaliza vita yakififia licha ya msisitizo wa Trump mnamo Agosti kwa viongozi hao kukutana.

Wakati wa Kongamano la Kiuchumi la Mashariki huko Vladivostok siku ya Ijumaa, Putin alisema kwamba hakuwa na nia ya kusafiri kwa mazungumzo na Zelensky lakini alikuwa tayari kwa mkutano na rais wa Ukraine huko Moscow. Aliongeza kuwa yuko tayari kwa mkutano kama huo na kwamba Moscow itatoa masharti ya usalama yanayohitajika kwa mkutano kama huo.