Jumanne , 18th Feb , 2020

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, leo Februari 18, 2020, imemkuta na kesi ya kujibu kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe, na ataanza kujitetea Machi 17 -20 mwaka huu.

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alivyowasili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi wakati kesi ya uchochezi namba 327 ya mwaka 2018, ilipofikishwa mahakamani hapo na kwamba maamuzi hayo yamekuja baada ya kupitia majumuisho ya pande zote mbili yaliyokuwa yamewasilishwa.

Baada ya kukutwa na tuhuma hizo za kujibu, Zitto alisema kuwa atakuwa na mashahidi 10 na ataanza kutoa utetezi wake kwa kiapo.
Katika kesi ya msingi Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi, anayodaiwa kuyatenda Oktoba 28, 2018, katika mkutano wa Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho.

Mbunge Zitto Kabwe alirejea nchini usiku wa kuamkia leo Februari 18, baada ya kufanya ziara ya Kidemokrasia nje ya nchi ikiwemo Marekani.