Jumamosi , 6th Oct , 2018

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) upande wa Profesa Ibrahim Lipumba amewakosoa baadhi ya makada waliokihama chama hicho kwa sababu ya migogoro na kuelekea Chama Cha Mapinduzi na kudai CCM ina migogoro lukuki kuliko iliyopo CUF.

Magdalena Sakaya, Mbunge wa Jimbo la Kaliua

Kwa mujibu Magdalena Sakaya, sababu zilizotolewa na Julius Mtatiro na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Liwale Zuberi Mohamed kuwa wamehama CUF sababu ya migogoro hazina mashiko badala yake amewatuhumu makada hao wamenunuliwa.

Sakaya amesema  “kusema kwamba wanahama CUF kwa sababu ya migogoro ni uongo, hakuna chama chenye migogoro kama CCM tena iko wazi mpaka viongozi wao wanaisema wazi, tena CCM ina migogoro lukuki tena kuliko CUF, ila tunaamini kupitia Profesa Lipumba migogoro itaisha maana huu si wakwanza”

“Kiufupi wao wamekubali kuwa bidhaa, wamenunuliwa na CCM lakini kwenye vyama vya siasa hakuna ambavyo havina migogoro, labda uende mbinguni ndio hautakuta migogoro kwa hiyo kwa mwanachama ambaye ni muumini wa CUF, hawezi kuhama kwa sababu ya migogoro. Ameongeza Sakaya.

Magdalena Sakaya ambaye ni mbunge wa Jimbo la Kaliua aliteuliwa kushika nafasi ya Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi wa (CUF) na Mwenyekiti wa Chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama nchini Profesa Lipumba baada ya madai ya kutofika ofisini kwa Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad.