Jumapili , 11th Oct , 2020

Wilaya ya Kisarawe imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuinua elimu ya mtoto wa kike zikiwemo za kutenga fedha kwa ajili ya kuwanunulia taulo za kike pamoja na kujenga shule ya sekondari ya bweni ya wanafunzi wakike.

Timu ya East Africa Tv na Radio ikimkabidhi Taulo za kike Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyofanyika kwenye shule ya Sekondari Minaki.

Mwegelo amesema  halmashauri imekuwa ikitenga fedha za kununulia taulo za kike ambapo mwaka jana ilitenga sh. milioni 4 na mwaka huu sh. milioni 3, jitihada ambazo pia zimekuwa zikiungwa mkono na EATV kupitia kampeni yake ya Namthamini.

Awali akifungua maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kisarawe, Mussa Gama, amesema kuwa wilaya ya Kisarawe bado inakabiliwa na tatizo la mimba za utotoni ambapo hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kudhibiti hali hiyo.

Kampeni ya Namthamini imefanikiwa kupatikana kwa taulo za kike zinazokidhi mahitaji ya wanafunzi wa kike 300 kwa mwaka mzima, pamoja na vifaa vingine vya shule.

Awali maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kisarawe kwa kushirikiana na EATV kupitia kampeni ya Namthamini yalianzia ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kisarawe hadi shule ya Sekondari Minaki.