Jumanne , 27th Oct , 2020

Ikiwa yamesalia masaa machache ya kufikia siku ya kupiga kura kwa ajili ya kuchagua vongozi nchini Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imesisitiza wananchi kuzingatia mambo muhimu yatakayomuwezesha kupiga kura ikiwemo kuwa na kadi ya mpiga kura.

Afisa Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Daniel Kalinga

Akizungumza leo katika kipindi cha Supa Breakfast Afisa Uchaguzi kutoka, NEC, Daniel Kalinga, amesema kuwa wale ambao hawana kadi ya mpiga kura wazingatie utaratibu uliotolewa na tume hiyo ikiwemo matumizi ya pass ya kusafiria, leseni na kitambulisho cha NIDA.

"Mambo muhimu ambayo mwananchi anapaswa ayazingatie na ayajue  ni ahakikishe anaanda kadi ya mpiga kura, mpiga kura ataenda yeye mwenyewe na kadi ya mpiga kura katika kituo cha kupigia kura alichojiandikisha” amesema Daniel Kalinga

Aidha Kalinga amewashauri wananchi wanaotarajia kupiga  kura ambao kadi zao zina matatizo waweze kutumia vitambulisho vilivoruhusiwa na Tume ya uchaguzi kuepuka matatizo.

"Kama kadi yampiga kura picha imefutika, majina hayaonekani basi nashauri mtu aweze kutumia utambulisho mwingine ili aweze kupata haki ya kupiga kura kwasababu akienda kituoni na kadi imefutika wasimamizi hawatoweza kumtambua" amesema Daniel Kalinga

Hata hivyo kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wananchi wataruhusiwa kupiga kura katika eneo walilojiandikisha kwa ajili ya upigaji kura na si vinginevyo huku wakitakiwa kufika na vitambulisho vitakavyowawezesha wasimamizi kuwatambua.