Jumatatu , 12th Oct , 2015

Msanii Shetta ambaye pia ni mmoja wa majaji wa mashindano ya Dance100% yaliyofikia finali zake siku ya jumamosi Tarehe 10 oktoba, amesema mashindano hayo yanarudisha hadhi ya wachezaji ambayo walikuwa nayo.

sheta ameyasema hayo kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, na kueleza kwamba siku za nyuma wasanii wa kucheza walikuwa hawathaminiwi, lakini kutokana na mashindano hayo kuteka hisia za watu wengi, imesaidia kuwarudishia heshima na kubadilisha maisha yao.

"East Africa TV wanavyorusha shindano kama hili, uthamani unaongezeka kwa sababu mwanzo kabisa tulikuwa si tuna dance heshima ilikuwepo, lakini hapa kati ikaja ikavurugika dancer hana thamani na vitu kama hivyo, lakini hata sisi wasanii wakubwa tunavyo waalika Dancers tunafanya nao show, tunawapa ajira maisha yanabadilika", alisema Sheta.

Nao washindi wa mashindano hayo ambao ni kundi la WD, wamewataka vijana kuwa na uthubutu wa kufanya vitu na kutokata tamaa wakihofia kushindwa.

"Namshukuru Mungu baada ya kutajwa washindi wa Dance 100% 2015, kwa sababu tumeshiriki ndani ya miaka mitatu bila mafanikio, lakini mwaka huu tumechukua washindi wa kwanza, kitu tulichoangalia ni ubunifu, usikubali kufanya kitu ambacho mwenzako amefanya au mtu mwengine amefanya, kupigana kwamba usikubali kusema hiki kitu mi sikiwezi", alisema Omary ambae ni mmoja kati ya washiriki wa kundi la WD.