Jumatatu , 12th Oct , 2015

Mashindano makali ya kucheza yaliyojizolea umaarufu mkubwa Afrika Mashariki Dance 100% 2015 yanafikia tamati jumamosi hii, ambapo mshindi wa fainali hizi mwaka huu atabeba kitita cha shilingi milioni 5 za Tanzania pamoja na zawadi nyingine.

Akipiga stori na mwandishi wa habari, mtayarishaji wa kipindi cha Dance 100% kinachorushwa na EATV kila jumamosi saa kumi na mbili na nusu jioni Ndimbuni Msongole, amesema fainali za mwaka huu zitakua na mvuto kwani ni makundi matano tu yamebaki kati ya makundi hamsini.

“Mwaka huu kutakua na good show (onyesho zuri) watu wategemee vitu vizuri kwani hakuna utabiri nani atakua mshindi makundi yalikua hamsini, lakini sasa yamebaki matatu kwa hiyo washiriki watatumia uwezo wao binafsi,” alisema Ndimbuni.

Naye mtangazaji machachari wa mashindano haya ya Dance 100% yanayoandaliwa na East Africa Television na East Africa Radio, TBway 360 amezungumzia tofauti ya fainali za mwaka huu na miaka iliyopita.

“Kuna tofauti kati ya mashindano ya miaka ya nyuma na mwaka huu kwa sababu makundi mengi yamerudi baada ya kushiriki mashindano ya miaka iliyopita hivyo washiriki wengi wana uzoefu mkubwa hali inayoleta fainali yenye ushindani zaidi,” alifunguka mtangazaji huyo.

Makundi yaliyofanikiwa kuingia fainali ni fainali za Dance 100% 2015 ni The WD, Team Makorokocho, Best Boys Kaka Zao, The Winners Crew pamoja na Team ya Shamba. Fainali hizo zitatimua vumbi jumamosi hii ya tarehe 10 saa nane mchana katika viwanja vya Don Bosco Oysterbay Jijini Dar es Salaam.