Jumatatu , 21st Oct , 2019

Muimbaji wa nyimbo za Injili hapa nchini, Goodluck Gozbert, amesema kuwa hakuwahi kutarajia hata siku moja, kama wimbo wake ungeweza kuchezwa Ikulu wakati wa shughuli ya uapishwaji wa viongozi.

Akizungumza leo Oktoba 21, 2019, na EATV&EA Radio Digital, ikiwa ni masaa machache tu yamepita tangu wimbo wake ulipotumika Ikulu, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, akiwaapisha viongozi, Goodluck amesema kuwa kitendo hicho kimemuinua katika viwango vya juu na kuwataka viongozi wateule wafuate nyayo za Dkt Magufuli.

 “Mimi sijawahi kuzoea vitu, kusema kweli nilistuka, nikawaza ni nani aliomba huo wimbo, ilikuwaje wimbo kuchezwa Ikulu, kwanini huo wimbo na hadi Asubuhi hii bado nawaza, unajua wimbo kusikika Ikulu sijawahi kuzoea licha ya kuwa na mimi nilishawahi kuitwa Ikulu, na nikaimba lakini bado kimeendelea kuwa kitu kikubwa kwangu na ninamshukuru Mungu juu ya hicho’’ amesema Goodluck.

Aidha kupitia wimbo wake huo wa ‘Hauwezi kushindana na wanadamu’ na maneno aliyoyazungumza Rais Dkt John Pombe Magufuli, siku ya jana ya Oktoba 20, 2019, Goodluck amewatia moyo viongozi wote wateule na kwamba wafuate nyayo zake za utendaji wake wa kazi na wasiwe watu wa kusikiliza maneno kama yeye anavyofanya.