Alhamisi , 31st Oct , 2019

Dada wa mchekeshaji Idris Sultan, Lulu Diva, amesema hadi sasa wamekwishampata Mwanasheria ambaye atamsaidia mdogo wake kupata dhamana, baada ya usiku wa kuamkia leo kujisalimisha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, leo Oktoba 31, 2019, Lulu Diva licha ya kupata kigugumizi juu ya namna ya kuzungumzia suala la ndugu yake kulala polisi, aliomba aachwe kwa muda kwa kuwa hata yeye haelewi hatma ya suala hilo.

"Kwakweli siwezi kuongela chochote kwa sababu mpaka sasa hivi kaka yangu yupo ndani na sijajua inakuaje, yupo Polisi Central, bado hatujapata taarifa yoyote, ndiyo tupo hapa na Mwanasheria kwa ajili ya kufuatilia kila kitu, mimi sifahamu naombeni mniache sijiskiii, siwezi na sipo katika 'mood' ya kuongea, tupo katika mipango ya kumsaidia tuone anatokaje ndani" amesema Lulu Diva.

Jana Oktoba 30, 2019, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,alimuagiza msanii huyo kujisalimisha katika kituo chochote cha polisi na kwamba maelezo yote angeyakuta huko, baada ya kuhariri picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, na kuweka sura yake.