"Manesi wapunguze kuchamba" - Miss Bella

Jumatatu , 13th Jan , 2020

Msanii kutoka kundi la Scorpion girls, Miss Bella, amedai kuwa madaktari wa hospitali za Serikali wapunguze kuchamba na ukali wa maneno, wakati wanatoa huduma kwa wagonjwa wao.

Picha ya Miss Bella

Miss Bella amefunguka hayo kupitia kipindi cha Mama Mia cha East Africa Radio, kinachoruka siku ya Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia 4:00 asubuhi hadi 6:00 mchana, ambapo wamezungumzia mada ya je ni kweli mwanamke akishajifungua anapoteza mvuto?.

"Wanaosema mwanamke aliye na mtoto anapoteza mvuto hana akili, hakuna mwanaume mwenye furaha kama aliyekuwa na mwanamke ambaye tayari ana mtoto, mbona mimi nipo vilevile na nina mtoto tena nina mpango wa kuijaza dunia" amesema Miss Bella.

Aidha mrembo huyo ameongeza kusema "Nina malalamiko kwa madaktari, kuna mtu aliniambia nikitaka kujifungua niende Hospitali za Serikali nikaenda ila nikakutana na kichambo hatari, siendi tena Hospitali za Serikali bora nikatoe pesa nyingi kwenye hospitali binafsi".

Pia ametoa ushauri kwa wasanii wenzake ambao wanaogopa kupata watoto kwa kusema, "Kuzaa sio kuzeeka mwisho wa siku sanaa zinapita, mnatoa sana mimba na umri unaenda nawashauri mzae jamani, unajiita staa wakati hauna mtoto na tabia zenu za ku-fake maisha wakati maisha yenu tunayajua mnatia aibu".