Ijumaa , 21st Aug , 2020

Mchekeshaji Mboto Haji  amemtambia msemaji wa Simba Haji Manara kwa kusema safari hii "litakufa toto la jitu" endapo wakikutana kwenye ligi pia hawezi kubishana naye kwa sababu yeye ni "Lopolopo Fc" yaani mropokaji.

Kulia kwenye picha ni Mboto Haji, kati mchezaji Benard Morisson na kushoto ni Msemaji wa Simba Haji Manara

Mboto Haji ambaye ni shabiki kindakindaki wa timu ya Yanga amesema kinachompa ujasiri ni usajili mkubwa walioufanya, kikosi kizuri pia hawatakuwa na shaka wala hofu ya jambo lolote.

"Natarajia makubwa sana kwa Yanga, sitaki kumzungumzia sana Haji Manara kwa sababu yule ni kaka yangu maana kuna radhi yake ila yeye ni lopolopo fc, ninachokiogopa kwake ni kupata laana japo kaka yangu anaropoka sana" amesema Mboto Haji 

Aidha mchekeshaji huyo ametoa fumbo ambalo linamlenga mchezaji mpya wa Simba ambaye ametoka timu ya Yanga.

"Ndugu yetu amepotea ana matatizo kidogo ya akili na tumeshatoa taarifa polisi na nguo ambazo ameondoka nazo tunazijua, ila chizi huwa haponi ila anapata nafuu ila siku moja ndugu zake atatutafuta maana dawa zake amezisahau"