Nipsey afariki dunia

Jumatatu , 1st Apr , 2019

Rapper Nipsey Hussle wa nchini Marekani ameuawa kwa kupigwa risasi alfajiri ya leo, baada ya kuvamiwa na watu wenye silaha kali.

Nipsey alivyoshambuliwa

 

Taarifa kutoka Los Angeles nchini Marekani zinasema kwamba tukio hilo limetokea nje ya duka lake la nguo, ambapo walikuja watu wakiwa kwenye gari na kuanza kummiminia risasi kadhaa zilizochukua uhai wake wakati akikimbizwa hospitali.

Kwenye tukio hilo watu wengine wawili wamejeruhiwa, kutokana na risasi zilizokuwa zikipigwa bila mpangilio.

Nipsey Hussle ambaye jina lake halisi ni Ermias Davidson Asghedom alikuwa na miaka 33, na alikulia Kusini mwa Los Angeles akiwa ni mwanachama wa kundi la vijana wa mtaani (Street gang) la Rollin 60s.

Muda mfupi uliopita rapper huyo aliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa twiiter uliosema kwamba “kuwa na maadui wenye nguvu ni baraka”, jambo ambalo limehusishwa kuwa huenda alijua nini kinakuja kutokea kwake.

Nipsey ameacha mke na watoto wawili wa kike, huku akiwa na album moja iliyokuwa imetajwa kwenye tuzo za Grammy mwaka huu, kama album bora ya rap.

UPDATE: Polisi wa Los Angeles wamefanikiwa kumpata mtuhumiwa wa mauaji hayo, ambaye wamemtaja kwa jina la Eric Holder, mwenye miaka 29.

Polisi imesema kuwa Eric alifika dukani hapo akiwa na silaha kisha kuwafayatulia risasi Nipsey na wenzake, kisha kukimbilia kwneye gari ambayo ilikuwa ikiendeshwa na mwanamke ambaye mpaka sasa hajajulikana.

Rapper Nipsey akiwa na mke wake