Kwa upande wa wanamuziki wa Hip Hop miongoni mwao wanaaminika kuwa ni watu wenye akili na ufahamu wa hali ya juu kwani kupitia muziki wao mara kadhaa hutoa mwelekeo mkubwa (ieleweke sio mara zote) na kumuonyesha mtu tatizo na namna ya kulitatua kwa usahihi.
Hip Hop ni kichocheo cha ubunifu na daima muelekeo halisi wa utamaduni wa Hip Hop ni kuona haki inatendeka na usawa unakuwepo katika jamii, baina ya tabaka moja na tabaka lingine, muziki huu upo kwa ajili ya kumfanya kila mmoja atambue wajibu wake katika jamii na ndio maana hata ambapo wasanii hawa wakiomba ridhaa ya kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa viongozi jamii huwapokea vizuri.
Kwa hapa Tanzania kuna baadhi ya Nyota wa muziki wa Hip hop ambao wamewahi kupewa dhamana ya kuwaonyesha watu njia kwa vitendo (kiongozi) na kuleta ushawishi kwa watu na kufikia maendeleo yaliyotarajiwa.
Hawa ni baadhi ya nyota ambao ni viongozi Serikalini na wengine waliwahi kuwa kwa kipindi fulani;

Joseph Mbilinyi (Mr II Sugu) – Huyu ni mwanamuziki wa Hip Hop wa kwanza kabisa ambaye alifanikiwa kuchaguliwa na kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020.

Joseph Haule (Professor Jay) – Ni kama alikuwa akijitabilia hivi kuja kuwa kiongozi wa wananchi hapo baadae kupiti tungo zake kama ‘Ndio Mzee’, na 2015 hadi 2020 alikuwa Mbunge wa Mikumi.

Hamis Mwinjuma (Mwana FA) – Ni mtu mwenye karama na maarifa kuhusu uongozi na namna ya kuongoza, alianza kuwa kwenye bodi ya BASATA na baadae kwenye uchaguzi mkuu 2020 alichaguliwa na wananchi kuwa Mbunge wa Muheza.

Nickson Simon John (Nikk wa pili) – Ni moja kati ya vijana makini mwenye ndoto, uchu wa mafanikio na mwenye matamanio ya kuwabailisha mitazamo baadhi ya watu, mwishoni mwa wiki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, alifanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya zote nchini, ambapo katika teuzi hizo Nikk wa pili pia ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.
