Jumamosi , 3rd Dec , 2016

Maonyesho ya mitindo ya mavazi ya Swahili Fashion Week 2016 yameanza jijini Dar es salaam, ambapo wabunifu kutoka sehemu mbali mbali Afrika wamepata fursa ya kuonyesha ubunifu wao.

Maonyesho hayo ambayo yameanza siku ya tar 2 Desemba yataendelea mpaka tarehe 4 Desemba 2016, yamekuwa na mafanikio makubwa kutoa fursa kwa wabunifu kutoka nje ya mipaka ya nchi yao na kukutana pamoja kuonyesha vipaji vyao vya ubunifu.

Mmoja wa wabunifu kutoka Afrika Kusini Tshepo Mafokwane amesema amejisikia furaha sana kushiriki maonyesho hayo ya mavazi, huku akiwa na lengo kubwa la kutangaza mitindo ya Afrika na kuweza kujulikana dunia nzima.

"Its nice to be here, we want to show the world what we can do, African designs are beutiful we create to impress the world and i hope we will reach there.....Akimaanisha ( Ni vizuri kuwa hapa, tunataka kuwaonyesha dunia nini tunaweza kufanya, ubunifu wa Afrika ni mzuri na tunabuni ili kuwahamasisha watu, na nina imani siku moja tutafika", alisema Tshepo Mafokwane kutoka Afrika Kusini.

Naye mbunifu kutoka hapa Tanzania Jamila Vera Swai amesema amefurahishwa na maonyesho ya mwaka huu kwani kumekuwa na mwamko mkubwa kutoka kwa watanzania ambao wameongezeka kushuhudia maonyesho hayo, tofauti na siku za nyuma.

"Maonyesho ya mwaka huu kama ulivyooona, Watanzania sasa wana muamko ingawa sio mkubwa sana, tofauti na siku za nyuma walikuwa hata kuja kuangalia ni wachache wanaoweza kuja, lakini mwaka huu wamekuwa wengi kidogo", alisema Jamila Vera Swai.

Maonyesho hayo yataendelea mpaka tar 4 Desemba jijini Dar es salaam, ambayo pia yamepambwa na biashara za vitu mbali mbali vilivyotengenezwa na wabunifu wa mitindo, ikiwemo mavazi, viatu na vitu vya urembo.

Mbunifu Tshepo Mafokwane kutoka Afrika Kusini akionyesha ubunifu wake kwenye Swahili Fashion Week 2016