Jumamosi , 17th Nov , 2018

Msanii wa muziki wa kizai kipya AT amekosoa kitendo cha 'social lite' Vera Sidika kuimba muziki, huku akimtuhumu kuwa hawezi kuimba na badala yake anapiga kelele.

Akizungumza kwenye Friday Night Live ya East Africa Television, AT amesema mlimbwende huyo kutoka nchini Kenya, amefanya kazi hiyo kwa kuiga, lakini kwenye suala la kuimba hajui kabisa huku akimfananisha na nyuki na kuitaka Afrika Mashariki kutokaa kimya kwenye masuala kama hayo, kwani inaharibu muziki wake.

“Huyu dada amejikelelesha, video sio mbaya, audio production siyo mbaya, ila muimbaji kaimba vibaya, hakieleweki kinachoimbwa ni nini, hajatayarishwa wala hajajitayarisha kuwa msanii, inawezekana kaona tu Mobetto alitoa kazi yake na yeye akaona atengeneze, kuimba sio kujamba kila mtu anaweza, lazima heshima iwekwe mezani, hizo kelele ni mbaya, mimi siwezi kuita nyimbo”, amesema AT.

AT ameendelea kwa kusema kwamba ….. “Afrika Mashariki kama tutakuwa tunasapoti kwa wasanii wa aina hii, tutakuwa tunafeli maana hatuwezi kwenda mbele, lazima tuvisemee,  tutakuwa tunajikekelesha, kama nyuki anatengeneza asali, haina ushirikiano kabisa kati ya sauti na beat”.

Hivi karibuni Vera Sidika ameachia wimbo wake wa kwanza ambao unaaminiwa amemuimba aliyekuwa mpenzi wake Otile Brown unaojulikana kwa jina la 'Nalia',  huku mwenyewe akisema kwamba wimbo huo unatokana na maisha yake halisi.