Alhamisi , 22nd Sep , 2016

Kampuni ya mtandao wa simu za mikononi nchini Tanzania, Vodacom leo imetoa elimu juu ya matumizi sahihi ya simu kwa washiriki wa fainali za shindano la Dance100% 2016 katika makao makuu ya Vodacom Jijini Dar es salaam.

Meneja wa idara ya huduma kwa wateja Vodacom , Willynevilline Msamo, akitoa maelezo kwa wawakilishi wa makundi yanayoshiriki fainali ya Dance100%

Akizungumza na washiriki hao ambao wametembezwa katika vitengo mbalimbali vinavyohudumia wateja wa kampuni hiyo, Meneja wa idara ya huduma kwa wateja Vodacom , Willynevilline Msamo amesema watumiaji wa simu wanatakiwa kuwa makini hasa katika lugha pamoja na kutuma na kupokea fedha kwani tatizo lolote likitokea ni rahisi kwa mhusika kupatikana.

'Tuzitumie simu zetu na mtandao wa Vodacom kwa manufaa mazuri, tusitukane watu tukidhania hatuwezi kupatikana au kuiba kwa kutumia mtandao , tukiamini tutakuwa salama, malalamiko yakitufikia ni rahisi sana kukupata sehemu ulipo” Amesema Msamo.

Wakati huo huo Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania,Matina Nkurlu amewataka vijana wanaoshiriki shindano hilo kutokukata tamaa kwani , juhudi na malengo ndiyo chanzo kikubwa cha mafanikio katika maisha.

Kwa upande wa mmoja wa waratibu wa shindano hilo kutoka EATV Brendansia Kileo amesema maandalizi ya shindano hilo yamekamilika watu wajitokeze kwa wingi siku ya Jumamosi hii, tarehe 24 viwanja vya Don Bosco Osterbay Jijini Dar es Salaam kuanzia saa nne asubuhi.

Aidha kwa upande wake Afisa Msaidizi wa Bidhaa na Masoko kutoka kampuni ya Coca- Cola Mariam Senziga amesema kampuni ya Coca -Cola inafurahishwa namna vijana wanavyojituma katika sanaa na kusisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kusapoti mawazo chanya yanayoibua vipaji.

Shindano la Dance100% 2016 linafikia tamati kwa mwaka huu Jumamosi ambapo matukio yote yanaoneshwa na EATV pekee kila Jumapili saa moja jioni na kudhaminiwa na Vodacom na Coca- Cola.

Tags: