Mimi ndoa ilinishinda - Bahati Bukuku

Jumatano , 18th Jan , 2017

Mwanamuziki mkongwe wa nyimbo za Injili Bahati Bukuku amefunguka na kuweka wazi kuwa ndoa ilimshinda na kusema katika harakati za maisha yeye alipishana na aliyekuwa mume wake kufikia hatua ya kutengana na sasa kila mmoja anaishi kivyake.

Bahati Bukuku akiwa Kikaangoni

 

Bahati Bukuku akizungumza LIVE kwenye Kipindi cha Kikaangoni kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV, alisema wimbo wake wa 'Dunia haina huruma' si kama alimuimbia huyo aliyekuwa mume wake bali ni kisa cha kweli kilichotokea lakini siyo kwenye ndoa yake na kwamba mambo hayo yalikuwa hayafanywi na huyo aliyekuwa mumewe.

"Aliyewahi kuwa mume wangu hakufanya hilo tukio ila kile kisa ni kweli kilitokea sehemu, lakini aliyekuwa mume wangu hakuwa na matatizo haya, ila tu katika harakati zetu za maisha kuna kupishana hivyo nilipishana naye tu. Siwezi kuongea uongo kwa mtu aliyekuwa mume wangu, hata nikiandika kitabu siwezi kuruka hili popote nikisimama nitasema niliolewa ndoa ikanishinda" alisema Bahati Bukuku 

Kuhusu skendo kuwa ndoa nyingi za "watu wa dini" hazidumu, Bahati amesema wanaume wengi wanakosea kufikiri kuwa wakioa wanawake ambao ni watu wa dini au watu wa injili kama yeye, wanakuwa wameoa watu wasio na makosa..

"Wengi hudhani ukioa mtu wa kanisani umeoa malaika ambaye hakosei, sasa wakishaanza maisha anakuta tofauti, hapo ndipo ndoa inaweza kuvunjika, jamani hata sisi ni binadamu pia" Alisema Bahati

Baadhi ya mashabiki walitaka kujua endapo alipata watoto katika ndoa hiyo, ambapo Bahati alikataa kuongea chochote kuhusu yeye kuwa na watota au la, na kusema kuwa hayuko tayari kuongea chochote huku akisema kuwa ana watoto wengi

"Hili swala la watoto sitaki kuzungumzia, mimi nina watoto wengi tu, kwahiyo kwenye ndoa yangu nisingependa kuongelea swala la watoto" alisema Bahati

Mbali na hilo Bahati Bukuku anasema watu ambao walimzushia kifo ni watu wake wa karibu ambao anafanya nao kazi na huenda walifanya hivyo ili kutaka kumpunguzia mashabiki wake.

"Walionizushia kifo ni watu ambao nafanya nao kazi, walidhani watanipunguzia mashabiki lakini pia ni kazi ya shetani hiyo, hivyo walijifanya ile taarifa imeanzia Congo lakini ni wa hapahapa ila mamlaka za mawasiliano bado zinaendelea kufuatilia ingawa mpaka sasa tayari wameshafahamika" alisema Bahati Bukuku 

Katika hatua nyingine, Bahati amesema hivi sasa anaandaa movie ambayo pia itakuwa na lengo la kuinjilisha, na kufikisha ujumbe wa Mungu kama ambavyo amekuwa akifanya kwenye uimbaji.

"Kwanza kabla sijatoa wimbo mpya, natoa filamu yangu mpya inayoitwa 'Mwalimu wa Ndoa', ambayo baada ya wiki moja itakuwa madukani, niliipeleka BASATA, tayari wameshaipitia, ina mafundisho mengi mazuri kuhusu ndoa, nawashauri wanawake, mabinti wote waitafute" Amesema Bahati huku akisita kutaja mastaa walioshiriki katika movie hiyo.