Jumatano , 10th Apr , 2019

Kama una imani ndogo unaweza ukashindwa kuiangalia picha ya mtoto Hope akiwa anapewa maji ya kunywa na raia wa kigeni akiwa amechuchumaa, kwa jinsi alivyodhoofu kwa njaa na maradhi huku mwili wake ukiwa haujavalishwa kitu chochote.

Mtoto huyu alikutwa akishangaa barabarani katika mji wa Uyo nchini Nigeria ambako ndio kulikuwa makazi yake, baada ya familia kumtenga na kumnyanyapaa wakiamini ni mchawi.

Msamaria mwema amuokoa Hope

 

Alikuwa hana hata miaka miwili wakati akitelekezwa mtaani katika moja ya mji nchini humo, huku wapita njia wakimrushia mabaki ya vyakula, jambo ambalo lilimgusa mwanamke mwenye asili ya Denmark, Anja Ringgren Loven, ambaye alimsogelea karibu, akachuchumaa na kumpa maji ya kunywa, kisha akamviligia blanket kumsitiri.

Anja hakuishia hapo, akampeleka hospitali ambako aligundulika kuwa na minyoo, kisha akapatiwa tiba huku akibadilishwa damu mara kadhaa ili kusafisha baadhi ya bakteria walioathiri afya yake.

Taratibu afya ya mtoto huyo ikaanza kutengemaa, akapewa jina la Hope, na kisha akachukuliwa rasmi na Anja, akampeleka kwenye kituo chake cha kulelea watoto walioathiriwa na mambo mbali mbali ikiwemo kutengwa na familia zao kwa sababu moja ama nyingine, na waliokosa wazazi.

Hope akiwa na Anja hospitali

Anja ambaye yuko barani Afrika akisaidia jamii katika kituo cha malezi kwa watoto, aliamua kuomba msaada zaidi wa matibabu ya Hope, na kupata muitikio mkubwa kutoka sehemu mbali mbali duniani, ambapo alipata zaidi ya dola milioni 1 iliyosaidia kuanzishwa kwa hospitali ndogo kituoni hapo kwa ajili ya jamii.

Mtoto Hope

Mtoto hope akiwa ameshapata afya nzuri

Hope ameendelea kuishi kituoni hapo na wenzake waliokumbwa na mkasa kama wake, na leo hii ikiwa ni miaka mitatu imepita, amekuwa mtoto mwenye kuvutia machoni, huku akiwa na tabasamu kubwa la matumaini mbele yake, pia akiwa ni tegemeo kubwa kwa wenzake kituoni hapo kutokana na kuwa na uwezo mkubwa kwenye michezo.

Mtoto Hope

Mtoto Hope alivyo sasa