Mke wa Chris Mauki atoa neno kwa wanaume

Jumamosi , 6th Jun , 2020

Mshauri wa Mahusiano, Familia na Malezi ambaye pia ni mke wa Mshauri wa masuala ya Kisaikojia Chris Mauki, Miriam Mauki amesema kuwa sababu kubwa inayopelekea wanaume kutembea na wasichana wa kazi ni kutokana na kwamba wasichana hao ni wanyenyekevu kuliko hata wake zao.

Mshauri wa Mahusiano, Familia na Malezi, Miriam Mauki.

Miriam ameyabainisha hayo leo Juni 6, 2020, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio, na kuongeza kuwa wanawake wengi wanapokuwa na wasichana wa kuwasaidia kazi huwa wanajisahau kutekeleza majukumu yao kwa kiasi kikubwa na badala yake wanabaki kushinda kwenye mitandao badala ya kuwahudumia waume zao.

"Mahusiano ya mapenzi kati ya Dada wa kazi na Baba, yanakuja kwa sababu ya unyenyekevu na mwanaume anapenda mwanamke mnyenyekevu, mara nyingi unakuta aliyeolewa anajisahau, hivyo mwanaume anaona Dada anamheshimu kuliko mkewe hivyo anamlipa fadhila" amesema Miriam.

Aidha Miriam ameongeza kuwa wanaume wanapofanya hivyo, siyo kwamba wanakuwa wanawapenda bali husukumwa na hisia za unyenyekevu wanaoupata, "Baba anapoanzisha mahusiano na msichana wa kazi siyo kwamba anampenda, lakini ule unyenyekevu unamvutia hisia za kuwa naye na anapomaliza haja zake anabaki kumuangalia kama mtu fulani tu, hata ukiangalia kwenye Guest House anayetangulia ni mwanaume kwa sababu hawezi kuvumilia kukaa pale sababu ile presha imeshaisha".