Nabii Tito aibuka tena, akiri kutumika kuangamiza

Jumatano , 1st Mei , 2019

Mtanzania mmoja anayejulikana kwa jina la Tito Machibya maarufu kama 'Nabii Tito', ameibuka tena na kudai kwamba kwa sasa yeye ameokoka, na kwamba Roho Mtakatifu ndiye anamuongoza kwenye maisha yake kwa sasa.

Akifunguka hayo Nabii Tito amesema kwamba kwa sasa anasali katika kanisa la BCIC lililopo Mbezi Jogoo jijini Dar es salaam chini ya Mchungaji Sylvester Gamanywa, huku akikiri kuwa kabla hajaokoka, shetani alimtumia sana kuangamiza maisha ya watu kwa kutoa mahubiri ya kupotosha.

“Unajua kwa sasa nimeamua kuokoka kwa sababu kule nilipokuwa, nilikuwa nikitumiwa na shetani na nimewaangamiza watu wengi kwa ushawishi wangu. Mimi nina akili yangu timamu, shetani alinitumia vibaya ndiyo maana nikawaangamiza na watu wengine, kwa sasa nimempokea Yesu Kristo na nimeamini kuwa yupo kweli,” amesema Nabii Tito.

Nabii Tito alipata umaarufu kutokana na mahubiri yake yenye kupotosha kusambaa mitandaoni hadi kufikia kukamatwa na polisi, lakini badaye alikuja kujulikana kuwa na matatizo ya akili, na kuachiwa huru.