Jumatano , 1st Dec , 2021

Veronica Lyimo, ni mwaamke anayeishi na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, ambapo amesema kwamba kwa mara ya kwanza alipojigundua na hali hiyo hakuweza kuikubali na badala yake alianza kujinyanyapaa mwenyewe.

Veronica Lyimo, anaishi na VVU

Kauli hiyo ameitoa hii leo Desemba 1, 2021, kwenye kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, ikiwa leo Dunia inaadhimisha siku ya UKIMWI Duniani, ambapo kitaifa maadhimisho haya yanafanyika mkoani Mbeya.

"Mimi nilipogundulika naishi na maambukizi ya VVU mwaka 2015 nilijinyanyapaa mwenyewe, hali ambayo ilipelekea hata ule unywaji dawa na kupata huduma za kiafya ikawa ngumu kwa upande wangu," amesema Veronica.

Aidha, ameongeza kuwa, "Baada ya Mjomba wangu kuniambia kwamba kuna maisha baada ya VVU akanikutanisha na majukwaa tofauti ya wanawake, na kuingia rasmi kupambana na hali ya kujinyanyapaa mwenyewe na nikagundua sipo peke yangu".