Alhamisi , 12th Sep , 2019

Utafiti wa miaka ya karibuni katika anga za juu, umeonesha uwepo wa sayari nyingine nje ya mfumo wetu wa jua (Solar System), ambazo zinatajwa kuwa na uwezo wa kuruhusu uhai kwa wanyama na mimea lakini ugumu umebaki kuweza kuzifikia.

Picha ya sayari tofauti tofauti

Unaambiwa kama chombo kitaweza kwenda spidi ya maili 35,000 kwa saa, itachukua miaka 40,000 kuweza kuikaribia sayari mojawapo, lakini inaelezwa uwepo wa ugumu wa kupita hata karibu ya Sayari hizo sababu zikitajwa ni uwepo wa mgandamizo mkubwa wa hewa pamoja na gesi nzito.

Utafiti mwingine wa hivi karibuni umegundua uwepo wa unyevu nyevu wa maji maeneo ya Sayari hizo, hivyo kuongeza uwezekano wa kuruhusu uhai kwa wanyama na mimea japo hiyo haitoi picha moja moja kwa sababu uwepo wa uhai hautegemei uwepo wa kitu kimoja bali vitu vingi.

Unyevu nyevu wa maji umegundulika katika sayari ya K2-18b ambayo kiumbo ni kubwa zaidi ya Sayari ya Dunia, lakini ina mfanano wa ukaribu wa hali ya hewa huku kukihisiwa kuwepo pia kwa vyanzo kama Bahari, Maziwa na Mito.

Mpaka sasa zimegundulika zaidi ya Sayari 2,000 ambazo zipo nje ya mfumo wetu wa Jua (Solar System), lakini imebaki kuwa ndoto kuzifikia sababu ya teknolojia iliyopo pamoja na ufinyu wa tafiti kuhusu maeneo hayo.