Jumatatu , 4th Jan , 2021

Kocha wa kikosi cha Chelsea, Frank Lampard amesema sababu za timu yake kuboronga kwa siku za hvi karibuni ni kutokana na kukosa muunganiko baada ya ujio wa wachezaji wengi wapya  na mchanganyiko wa wachezaji wenye umri mdogo wasio na uzoefu.

Kocha wa Chelsea Frank Lampard.

Lampard ameyazungumza hayo kwa ghadhabu kubwa baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Manchester City kwenye ligi kuu ya England na kuishuhudia Chelsea ikiwa na mwenendo mbaya mikononi mwake.

Mabao ya City yamefungwa na Ilkay Gundogan, Kevin De Bruyne na Phil Foden huku moja la kufutia machozi la Chelsea likifungwa na Callum Hodson Odoi. 

Baada ya kichapo hicho Chelsea imedondoka hado nafasi ya 8 wakiwa na jumla ya alama 26 alama 3 tofauti na Arsenal.  

Lampard amesema “ Matarajio ni tofauti mwaka huu na namna watu wanavyohusisha kiasi cha pesa tulichotumia. Tumetumia pesa nyingi sana lakini uhalisia ni kwamba wachezaji wana umri mdogo na hawajacheza pamoja kwa muda mrefu”.

“Ni kwa mara ya kwanza Hakim Ziyech, Christian Pulisic na Timo Werner kucheza pamoja, na kama tunatarajia muunganiko wa wachezaji hawa watatu leo hii kuwa sawa na Bernardo Silva, De Bruyne na Sterling basi matarajio hayo hayana uhalisia”.

Chelsea tayari wamepoteza michezo 4 kati ya 6 ya mwisho ya EPL na kufikisha alama 26 na wakidondoka mpaka nafasi ya 8 licha ya mwanzoni mwa mwezi disemba kuwa kileleni mwa msimamo  wa EPL.

Kuboronga huko kwa Chelsea kumemfanya kocha Frank Lampard kuwa kocha mwenye uwiano mdogo  1. 67 wa kupata ushindi ukiwa ni uwiano mdogo zaidi kuliko baadhi ya makocha waliotangulia Mauricio Sarri, Claudio Ranieri, Andres Villas Boas na Roberto Di Matteo.

Kuhusu Chelsea kuwepo au kutokuwepo kwenye mbio za Ubingwa Lampard amesema “Baada ya ushindi dhidi ya Leeds Utd nilihisi sisi sio miongoni mwa timu zinazowania Ubingwa. Na sasa nasema kiuhalisia kwamba ujenzi wa timu unakuja na maumivu yake makali”. 

“Nakumbuka Pep Guardiola alipitia hatua hii kwenye msimu wake wa kwanza na Man City na sasa tunajua stori yake. Unajenga timu kupitia mapambano na uthubutu mkubwa”. Tunajua stori ya Man City na Liverpool japo siwalinganishi sana na sisi.

Mwenendo wa Chelsea kuboronga umewafanya baadhi ya mashabiki wa Chelsea kufikiria huenda kocha huyo akatimuliwa kazi licha ya Lampard kusema hawezi kujibia kama kibarua chake kipo salama  kwasababu bodi ya klabu ndiyo wenye mamlaka ya kujibia hilo.