
Mohamed Salah akiwa na shabiki kipofu, Mike Kearney (kulia) pamoja na ndugu yake (kushoto)
Shabiki huyo alionekana katika video moja akiwa katika uwanja wa Anfield pamoja na ndugu yake akishangilia kwa hisia kali licha ya kuwa hakuwa anauona mchezo huo hasa baada ya Salah kufunga bao katika dakika ya 34 ya mchezo.
Mchezo huo ulimalizika kwa Liverpool kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na kufanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, ambapo sasa imepangwa na Bayern Munich.
Akiongea baada ya kukutana na Mohamed Salah licha ya kutomuona kwa macho, lakini alikuwa akionekana mwenye furaha na alipoulizwa ni lini alianza kuishangilia timu hiyo, Kearney amesema, "nimeanza kuishangilia Liverpool tangu nilipojitambua na nimekuwa nikija kuiangalia timu hii uwanjani mwaka wa tano sasa".
Shabiki huyo pamoja na ndugu yake ambaye muda wote humsaidia kumtambulisha vitu mbalimbali, walitembelea katika uwanja wa mazoezi wa Melwood kushuhudia wachezaji wakifanya mazoezi, ambapo kabla ya mazoezi hayo kuanza wachezaji walipata wasaa wa kusaini jezi maalum ya shabiki huyo.