
Atletico wakiwa na faida ya bao la nyumbani katika nusu fainali ya kwanza nchini Hispania, Bayern walisawazisha kupitia mkwaju wa adhabu ndogo uliopigwa na Xabi Alonso kwenye mechi ya jana usiku iliyochezewa uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Arena.
Golikipa wa Atletico Jan Oblak aliokoa mkwaju wa penalti uliopigwa na Thomas Muller kabla ya mshambuliaji Antoine Griezmann kusawazisha na matokeo kuwa 1-1.
Robert Lewandowski alifunga bao la pili baada ya kupokea pasi ya mpira wa kichwa kutoka kwa Arturo Vidal huku Atletico wakishindwa kusawazisha baada ya mkwaju wa penalti uliopigwa na Fernando Torres kuokolewa na mlinda mlango Manuel Neuer.
Matokeo ya jumla ya nusu fainali hiyo yalimalizika sare 2-2 lakini Atletico Madrid wakasonga mbele kwa kuwa na bao la ugenini.
Sasa Atletico watakutana na mshindi wa mchezo kati ya Real Madrid na Manchester City utakaopigwa leo dimbani Santiago Bernabeu, katika fainali mjini Milan tarehe 28 Mei.
Chanzo BBC