Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Burundi alifunga bao hilo Dakika ya 17 kwa kichwa akimalizia Krosi ya beki wa kulia, Shomary Kapombe.
Kavumbagu sasa anatimiza mabao tisa katika mbio za ufungaji bora akifuatiwa na Rashidi Mandawa wa Kagera Sugar mwenye mabao nane na Abasalim Chidiabele wa Stand United mwenye mabao saba.
Na ushindi huo unaifanya Azam kutimiza Pointi 30 baada ya mechi 16 ikizidiwa pointi moja na vinara Yanga Sc ambao hata hivyo wamecheza mechi 15.
Katika mchezo huo, Refa Kennedy Mapunda aliwatoa nje kwa kadi nyekundu Richard Maranya wa JKT Ruvu na Salum Abubakar Sure Boy wa Azam Fc katika Dakika ya 59 baada ya kupigana.
Huo umekuwa mchezo wa kwanza kwa Azam Fc tangu imfukuze kocha wake, Mcameroon, Joseph Marius Omong huku timu ikiongozwa na Mganda, George Best Nsimbe.
Kwa upande wa Coastal Union imelazimishwa sare nyumbani kwa kufungana mabao 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Coastal ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya sita kupitia kwa Suleiman Kibuta kabla ya Atupele Green kuisawazishia Kagera Sugar dakika 52 akimalizia kona ya George Kavilla.
Coastal ikafanikiwa kuongoza tena kuongoza mchezo kwa bao la Rama Salim kwa Penati katika Dakika ya 67, kufuatia Kibuta kuchezewa rafu na beki wa Kagera, Ibrahim Job.
Hata hivyo Kagera, wakasawazisha kwa mara nyingine, Mfungaji Rashidi Mandawa baada ya kazi nzuri ya Erick Kyaruzi katika dakika ya 85 ambapo kwa matokeo hayo yanaifanya kila timu ijiongezee pointi moja.