Baada ya kuteuliwa, Jimmy Kindoki awapa onyo Simba

Jumatano , 11th Sep , 2019

Shabiki na mwanachama kindakindaki wa Yanga ambaye amejizolea umaarufu hivi karibuni mtandaoni, Jimmy Msindo maarufu kama 'Jimmy Kindoki' ameteuliwa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Hamasa ndani ya klabu hiyo.

Mjumbe wa Kamati ya Hamasa wa Yanga

Kamati hiyo yenye wajumbe 19 ni ya kudumu kwa ajili ya kuhamasisha kampeni mbalimbali ndani ya klabu hiyo ili iweze kufanya vizuri na kufikia malengo.

Akizungumza na EATV/ EA Radio Digital, Jimmy amesema kuwa sasa amepata rungu rasmi la kuisemea klabu hiyo mahali popote na kuahidi kupambana na mtu yoyote atakayethubutu kuichafua Yanga.

"Katika mwaka ambao uongozi wa Yanga umetenda haki ni huu, imempa nafasi mtu sahihi. Nilikuwa nafanya kazi nje ya mfumo na sasa nimeingia ndani rasmi, hata mashabiki wanafurahishwa kuona hiki kitu", amesema Jimmy.

"Wenzetu Simba wameumia sana kitendo cha sisi kubakia kwenye Klabu Bingwa Afrika na ndiyo maana kila siku wanahangaika kufanya kila kitu ili sisi tukwame. Sasa hivi wameufunga Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru wameweka vitu vyao, nawaambia wakavitoe", ameongeza Jimmy.

Kamati hiyo ya hamasa ya Yanga imeanza kufanya kazi hivi sasa kuelekea mchezo wa Klabu Bingwa Afrika kati ya Yanga na Zesco ya Zambia, utakaopigwa Jumapili, Septemba 14 katika Uwanja wa Taifa.

Tazama Interview nzima hapa chini alichokizungumza Jimmy Kindoki.