Balaa la majeruhi Yanga

Saturday , 12th Aug , 2017

Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Yanga Godfrey Mwashiuya ataukosa mchezo wa pili mfululizo katika mechi za kirafiki ikiwa leo Yanga itashuka dimbani dhidi ya Ruvu Shooting kwa ajili ya maandalizi ya msimu huu kufuatia jeraha linalomsumbua.

 

Mwashiuya kupitia katika ukurasa wake wa instagram amewaomba mashabiki wake na wadau wa soka kumuombea ili apone na kuweza kujiunga na kikosi chake kwenda kupambana ili kufanya vizuri katika msimu mpya wa ligi unaotarajiwa kuanza siku za hizi karibuni. 

"Naombeni maombi yenu jamani,  nasumbuliwa na mguu" - alisema kiungo huyo.

Aidha klabu ya Yanga itashuka dimbani dhidi ya Ruvu Shooting leo ikiwa ni mechi ya pili ya kirafiki katika uwanja wa Azam Complex, Chamanzi saa kumi Jioni. Yanga baada ya kumaliza mchezo wa leo kesho watakipiga tena na klabu ya Mlandege FC Zanzibar na baada ya hapo watakwenda visiwani Pemba kuweka kambi ya wiki nzima kujianda na mchezo wa ngao ya jamii utaokaofanyika Agosti 23 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.