Baraka The Prince akoshwa na Bball Kings

Jumanne , 14th Aug , 2018

Nyota wa Bongofleva Baraka the Price anayetamba na ngoma yake mpya 'Sina', ni miongoni mwa waliokoshwa na mashindano ya Kikapu ya Sprite Bball Kings baada ya kujionea game 3 ya nusu fainali kati ya Portland dhidi ya Mchenga Bball Stars.

Timu za Portland (nyeupe) na Mchenga Bball Stars (kijani) kwenye game 3 ya nusu fainali.

Akiongea na East Africa Television Baraka aliweka wazi kuwa michuano hiyo ni daraja zuri kwa vijana wa Kitanzania wenye vipaji kujiajiri na kufikia ndoto zao ikiwemo kucheza kwenye ligi kubwa nje ya nchi kitu ambacho kitasaidia kuinua wengine.

''Huu ni mchezo wenye pesa nyingi sana na unatoa mastaa wengi kwenye nchi za wenzetu, kwa hiki ambacho mmekifanya East Africa Television ni kitu kikubwa maana vijana wanapata kujulikana na kujipatia kipato kama hivyo bingwa anachukua milioni 10 na pia anakuwa ametangaza kipaji chake'', alisema.

Baraka pia alieleza kushangazwa na umati mkubwa wa mashabiki waliojitokeza kwenye viwanja vya Don Bosco kushuhudia game 3 ya nusu fainali ambapo Mchenga waliwalaza Portland kwa pointi 81 kwa 63. ''Nimehamasika kuja tena maana kumbe huku kuna mashabiki wetu wengi tu'', aliongeza.

Game za fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na kinywaji cha Sprite zitaanza kupigwa Jumamosi hii Agosti 18 kwenye uwanja wa taifa wa ndani ambap Flying Dribblers watakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars.