
(Baadhi ya wachezaji wa Barcelona wakihuzunika baada ya kipigo)
Wababe wa Uhispania, timu ya Barcelona imeondolewa kwenye michuano ya klabu bingwa barani Ulaya baada ya usiku wa jana kukubali kipigo ba 3-0 kutoka kwa Bayern Munich ya Ujerumani.
Jahazi la Barcelona lilizamishwa na Thomas Muller, Jamal Musiala na Leroy Sane’ ambaye alifunga kwa shuti la umbali mrefu na kumuacha mlinda mlango wa Barcelona Marc Andre Ter Stegen kukosa la kufanya.
Kocha mkuu wa timu hiyo Xavi Harnandez ameweka wazi kusikitishwa kwake baada ya mchezo huo na pia alikizungumzia kuwa sasa ni mwanza wa zama mpya huko Camp Nou.
"Mimi nina hasira. Huu ndio ukweli na inaniudhi. Tunapaswa kukabiliana nayo usoni. Hakuna kingine kwasasa zaidi ya kushinda. Zama mpya inaanza sasa. Tunaanzia sifuri,” amesema Xavi.
"Lengo la Barca ni Ligi ya Mabingwa, sio Ligi ya Europa. Lakini ukweli wetu wa sasa ni Ligi ya Europa na tunapaswa kwenda njia hii na kushinda. Hili ndilo lengo la Barca - kushinda kila mchezo na kushinda kila taji."
Mara ya mwisho Barcelona kutolewa kwenye hatua ya makundi ilikuwa miaka 20 iliyopita ambapo ilikuwa msimu wa mwaka 2003-2004 huku kocha wake wa sasa, Xavi Hernandez alikuwa mchezaji.
Wakati Barcelona ilipokuwa inatolewa msimu wa mwaka 2003-2004 wachezaji makinda wa sasa wakina Ansumane Fati, Pedri na Gavi walikuwa hawajazaliwa.
Barcelona imemaliza ikiwa nafasi ya tatu ikiwa na alama 7 nyuma ya Benifica wenye alama 8 na kinara Bayern Munich mwenye ushindi wa asilimia 100 kwenye michezo 6 akiwa na alama 18 huku Dynamo Kiev akishika mkia.
Kwa upande mwengine, timu 15 zimepatikana kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora huku mchezo wa Atalanta dhidi ya Villarreal umepangwa kucheza saa 3:00 usiku wa leo baada ya jana uwanja wa Atalanta kujaa mabarafu.
Timu zilizofuzu ni, Kundi A: PSG, Man City kundi B: Liverpool, Atletico kundi C: Ajax, Sporting CP kundi D: Real Madrid, Inter Milan kundi E: Bayern, Benifica F: Man Utd, na mshindi wa mchezo kati ya Atalanta na Villarreal leo.
Kundi G: Lille, RB Salzburg na kundi H: Juventus na Chelsea. Droo ya nani kucheza na nani kwenye hatua ya 16 bora itapangwa disemba 13 huku michezo ya mkondo wa kwanza itachezwa Februari 15 – 23, 2022.