Ijumaa , 3rd Aug , 2018

Nahodha wa Mchenga Bball Stars, Mohamed Yusuf, amefunguka kuwa ukubwa wa michuano ya Sprite Bball Kings inayoandaliwa na East Africa Television LTD na kudhaminiwa na kinywaji cha Sprite, unatosha kuwapa nafasi wachezaji ya kuonekana na pengine kucheza kimataifa. 

Mohamed Yusuf katikati akijadili jambo na wenzake wakati wa mchezo wao dhidi ya Portland.

Mohamed Yusuf ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum na kipindi cha East Africa Breakfast kupitia East Africa Radio, ambapo ameeleza kuwa mbali na zawadi wanazopata washindi lakini ukubwa wa michuano hiyo ndio kitu kingine kinachowafanya wajitume zaidi.

''Unajua kwenye michuano hii kila mchezaji anajitahidi kuonesha kiwango chake sio tu kwaajili ya kupata zawadi bali kutokana na ukubwa wa michuano hii watu wanawaza kupata nafasi ya kucheza kimataifa na ninaamini jambo hilo linawezekana'', - amesema.

Mbali na hilo Mohamed maarufu kama Mood, ameongelea 'game 2' ya nusu fainali ambapo amesema wanatarajia kukata tiketi ya fainali kesho akidai haoni kama wapinzani wao ambao ni Portland watawazuia haswa baada ya kushinda game 1 kwa pointi 70 dhidi ya 54.

Game 2 za best of three ya nusu fainali ya Sprite Bball Kings zitapigwa kesho Jumamosi Agosti 4 kwenye uwanja wa taifa wa ndani jijini Dar es salaam. Flying Dribblers baada ya kushinda 'game 1' kwa pointi 84 kwa 75 za Team Kiza watakipiga tena kutafuta nafasi ya fainali. Mchenga nao watakipiga na Potrland. Mechi zitaanza saa 10:00 jioni na hakutakuwa na kiingilio.