Jumatatu , 19th Feb , 2018

Mashabiki wa soka nchini Brazil jana wameshuhudia tukio lisilo la kawaida michezoni baada ya wachezaji tisa kuoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa 'Derby' kati ya  timu za Vitoria na Bahia, baada ya kutokea vurugu kuelekea mwisho wa mechi.

Vurugu hizo ziliibuka zikiwa zimesalia dakika 11 kabla ya mchezo huo kumalizika baada ya mchezaji wa Bahia kusheherekea goli akiwa ameisawazishia bao timu hiyo na kuwa sawa kwa mabao 1 - 1.

Kufuatia bao hilo alilofunga kwa Penati na kushangilia kwa mtindo ambao ulionekana kuwakera wachezaji wa timu mwenyeji ambayo ni Vitoria na kuanza kumshambulia kabla ya wenzake wa Bahia kuingilia kitendo ambacho kilipelekea mwamuzi kutoa kadi hizo na mchezo kuishia dakika ya 79.

Wachezaji sita wa wenyeji wa mchezo Victoria walipata kadi nyekundu za moja kwa moja huku wachezaji watatu wa timu ya Bahia nao walioneshwa kadi nyekundu hivyo kufanya mchezo usiendelee.

Refarii alilazimika kuahirisha mechi kutokana na taratibu za mchezo wa soka kuhitaji angalau wachezaji saba wa timu wawepo uwanjani.

Mahakama ya michezo ya Brazil inasubiriwa sasa kuamua juu ya hatua gani za kuchukua kufuatia vurugu hizo ambazo zilipelekea kuharibika kwa mchezo huo ambapo timu zilikuwa zimefungana bao 1-1.