Jumatatu , 31st Mei , 2021

Klabu ya Yanga na mchezaji wake Carlos Stenio Fernandez Guimares do Carmo maarufu kama 'Carlinhos' wamekubaliana kusitisha mkataba kuanzia sasa.

Kiungo mchezeshaji Carlos Carlinhos

Taarifa rasmi ya klabu ya Yanga imesema kiungo huyo mshambuliaji aliwasilisha maombi kwa uongozi na baada ya majadiliano na kwa kuzingatia maslahi mapana ya pande zote, uongozi wa timu umeafiki ombi lake.

Carlinhos aliondoka jana Jumapili ya tarehe 30/5/2021 jioni akielekea nyumbani kwao Angola, huku matatizo ya kifamilia yakitajwa kuwa ni chanzo cha kufikia maamuzi hayo ya kusitisha mkataba huo.

Carlinhos alijiunga na Yanga dirisha kubwa la usajili la usajili 2020 kwa mkataba wa mwaka moja na nusu, amekuwa na majeraha ya mara kwa mara katika msimu huu hali iliyomfanya kushindwa kutoa mchango kwenye timu ya wananchi ambayo ina kiu kubwa na ubingwa.

Japo kwenye mechi chache alizocheza ametoa mchango mkubwa sana ikiwemo kufunga magoli 3 kwenye ligi kuu na kutoa pasi msaada 'assist' 3 katika mechi 9 alizocheza akiwa na  Yanga, usahihi mkubwa wa matendo ya uwanjani ikiwemo uwezo wa kupiga pasi ndefu na faulo zikiwemo kona umeinufaisha sana timu hiyo.