Alhamisi , 28th Apr , 2016

Chama cha mchezo wa Darts [vishale] Tanzania kimesema maandalizi ya michuano ya ubingwa kwa nchi za Afrika Mashariki yatapigwa kwa siku mbili jijini Dar es Salaam katika maeneo ya Manzese yakishirikisha nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania.

Baadhi ya wachezaji wa mchezo wa darts [vishale] nchini wakichuana.

Michuano ya kimataifa ya mchezo wa Darts kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati yanataraji kufanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Aprili 30 mwaka huu na kuhitimishwa May Mosi mwaka huu katika ukumbi wa Moshi Bar Ulioko maeneo ya Tip Top Manzese jijini Dar es Salaam.

Tanzania ambao ni wenyeji chini ya Chama cha mchezo TADA wamesema maandalizi yote ya kiutawala na kimiundombinu yaemkamilika na tayari baadhi ya wachezaji kutoka nchi shiriki kama Uganda na Kenya wameanza kuwasili nchini na wengine wako njiani wakitegemewa kuwasili wakati wowote hii leo na kesho na kuanza mashindano hayo rasmi kuanzia saa 3 asubuhi ya jumamosi Aprili 30 mwaka huu.

Wakizungumzia mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka kwa kupokezana uwenyeji kwa nchi wanachama wa shirikisho la mchezo wa darts Afrika Mashariki EADF viongozi wapya wa TADA Mwenyekiti Wiston Asesya na katibu mkuu wake Subira Waziri wameomba wadau wa michezo nchini kote wawaunge mkono kwa hali na mali ili kufanikisha mashindano hayo makubwa ambayo yanafanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam huku pia wao wakiyasimamia kwa mara ya kwanza wakiwa kama viongozi wa mchezo huo taifa jambo ambalo amekiri litakuwan a changamoto kubwa sana kwao kwakuwa walikuwa wakiongoza vyama vya mikoa hapo awali na sasa wameingia katika kazi hiyo nzito hivyo ushirikiano unatakiwa kupewa nafasi ya kipekee ili kufanikisha jambo hilo kubwa.

Tanzania imeshawahi kuandaa michuano hiyo ya kimataifa ikifanyika katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Kagera na sasa inafanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam tena chini ya uongozi mpya wa chama cha mchezo wa darts [vishale] nchini TADA.