Jumatano , 9th Oct , 2019

Ligi ya soka maarufu duniani hivi sasa EPL italazimika kupoteza nafasi moja kati ya nne za moja kwa moja kushirki michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

Mabingwa wa Klabu Bingwa Ulaya 2018/19, Liverpool

Hiyo ni kutokana na mapendekezo mapya ya Shirikisho la Soka barani Ulaya UEFA juu ya kubadilisha muundo wa mashindano makubwa ngazi ya klabu barani humo pamoja na kutambulisha mashindano ya tatu ya vilabu.

La Liga, Serie A na Bundesliga pia zitaathiriwa na mfumo huo, ambapo kuanzia msimu wa 2024 ligi hizo zitatoa nafasi tatu za moja kwa moja kuingia katika makundi ya Klabu Bingwa Ulaya na watakaoshika nafasi ya nne watalazimika kuanzia katika mchujo.

"Nafikiri ligi kubwa zitaridhia endapo sheria itatumika kwa kuzingatia usawa. Mfano ukitoa nafasi kwa EPL kuingiza timu nne halafu Bundesliga ukawatolea nafasi moja, lazima tatizo litatokea", amesema Lars-Christer Olsson ambaye ni Rais anayewakilisha ligi 36 za bara la Ulaya.

Olsson amesema kuwa majadiliano ya mapendekezo hayo yatahusisha ligi zote kubwa.

Jambo lingine ambalo linatarajiwa kuwekwa mezani ni kuhusu mgawanyo wa mapato ya faida kwa klabu ambazo hazishiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, ambapo pendekezo lililopo ni la kuzipa mgawanyo hadi kufikia asilimia 25.

Wawakilishi wa ligi na mashindano mbalimbali ya Ulaya pamoja na klabu watakuwa na mkutano mwingine wa majadiliano mjini London wiki ijayo.