Jumamosi , 18th Aug , 2018

Kuelekea mchezo wa ngao ya jamii kati ya Simba na Mtibwa Sugar katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza hii leo, ifuatayo ni historia pamoja na washindi wa kombe hilo tangu kuanzishwa kwake.

Wachezaji wakichuana katika moja ya mchezo kati ya Simba na Mtibwa Sugar

Mchezo wa ngao ya jamii ulianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2001 kabla ya kuitishwa kwa miaka kadhaa na kurejea tena kuanzia mwaka 2009.

Mchezo wa kwanza uliikutanisha kati ya Simba na Yanga na hatimaye Yanga kuibuka mshinmdi wa kwanza wa kombe hilo kwa kuifunga Simba 2-1, mabao ya Yanga yakifungwa na Edibily Lunyamila na Ally Yussuph ‘Tigana’ huku bao pekee la Simba likifungwa na Steven Mapunda ‘Garincha’.

Tangu kuanzishwa kwa mchezo huo wa ngao ya jamii, Yanga na Simba ndiyo zinaongoza mpaka sasa kwa kushinda mara nyingi kuliko klabu zote, zikiwa zimeshinda mara 5 kila moja huku Mtibwa Sugar na Azam Fc zikiwa zimeshinda mara moja.

Historia ya karibuni kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka uliopita, Klabu ya Yanga imeshinda kombe hilo mara nne huku Simba ikishinda mara tatu na Azam Fc pamoja na Mtibwa Sugar zikishinda mara moja.

Simba inaelekea katika mchezo wa leo ikisaka kombe la sita huku Mtibwa Sugar ikisaka kombe la pili katika historia yao . Simba ikiwakilisha kama bingwa wa ligi kuu msimu uliopita huku Mtibwa Sugar ikiwakilisha kama bingwa wa kombe la shirikisho kwa msimu uliopita pia.