Alhamisi , 8th Jun , 2023

Mchezaji mpya wa klabu ya Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' amesema kuwa licha ya kusaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia klabu yake hiyo mpya lakini bado anaipenda timu yake ya Yanga ambayo alikuwa anaitumikia kwa muda mrefu.

Fei Toto ameyasema hayo leo Alhamis Juni 8, 2023 jijini Dar es salaam wakati anatambulishwa rasmi baada ya uongozi wa Yanga kukubali kumuuza Azam na amewashukuru viongozi wa Yanga pamoja na mashabiki kwa ujumla kwa kipindi alichokaa nao lakini bado anawapenda.

''Matarajio yangu ni makubwa na waahidi mashabiki  kuwa na furaha pindi wa Azam FC tunapocheza '' Feitoto amesema

 Kwa upande wa mtendaji mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' amesema wanamshukuru Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassani kwa kulimaliza Sakata hili la mchezaji dhidi ya klabu yake ya Yanga hivyo mchezo wa mpira ni umoja na ushirikiano.

Feisal Salum 'Feitoto' aliingia kwenye mgogoro na klabu ya Yanga baada ya kufanya jaribio la kuvunja mkataba jambo ambalo lilipelekea mvutano na iliyokuwa klabu yake hadi kufikishwa mbele ya kamati ya hadhi na sheria ya Wachezaji iliyoamuru Feisal arejee Yanga SC.