Jumapili , 22nd Jul , 2018

Timu ya mpira wa Kikapu Flying Dribblers imekuwa kinara kwenye pointi kati ya timu 4 zilizofuzu hatua ya nusu fainali ya michuano Sprite Bball Kings baada ya kupata pointi 100 kwenye mchezo wake wa robo fainali dhidi ya Water Institute.

Timu ya Flying Dribblers.

Mchezo huo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa taifa wa ndani Julai 21, 2018, ulishuhudia Flying dribblers ambayo msimu uliopita iliishia hatua ya nusu fainali kwa kuondolewa na walioibuka mabingwa Mchenga Bball Stars ikishinda vikapu hivyo 100 dhidi ya Water Institute hivyo kuwa na tofauti ya pointi 36.

Katika mbio hizo za nusu fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na East Africa Television LTD na kudhaminiwa na kinywaji baridi cha Sprite, nafasi ya pili imeshikwa na Team Kiza ambao waliwafunga DMI kwa pointi 82 kwa 47 hivyo kuwa na tofauti ya alama 35.

Mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars ambao kiwango chao kinaonesha wamepania kutetea ubingwa wao, wamekaa katika nafasi ya tatu baada ya mechi yao dhidi ya St. Joseph kumalizika kwa wao kushinda pointi 84 kwa 67 hivyo kuwa na faida ya pointi 17.

Timu ya Portland yenyewe ndio imekamilisha orodha ya timu 4 zitakazo pepetana kwenye nusu fainali baada ya kuwashinda wenye uwanja wao wa Temeke Heroes kwa pointi 83 kwa 70 katika mchezo uliokuwa na ushindani wa hali ya juu. Portland walijikusanyia faida ya pointi 13.

Droo ya hatua ya nusu fainali itafanyika Jumatatu ya Julai 23, na itaoneshwa moja kwa moja kupitia East Africa Television kupitia kipindi cha 5Sports na kusikika kupitia The Cruise ya East Africa Radio.