Alhamisi , 30th Jan , 2020

Klabu ya soka ya Simba imeibuka na ushindi dhidi ya Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara, jana Jumatano, Januari 29.

Meddie Kagere na kocha wa Yanga, Luc Eymael

Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa, ulishuhudia Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo, mabao ya Simba yakifungwa na Francis Kahata, Hassan Dilunga, na Meddie Kagere, huku mabao ya Namungo yakifungwa na Bigirimana Blaise na Lucas Kikoti.

Bao la tatu na la ushindi kwa Simba lililofungwa na Kagere ndilo lililozua gumzo kubwa miongoni mwa wadau wa soka, wengi wakisema ni la kuotea kwa jinsi ambavyo marudio ya video yalivyoonesha.

Wadau wengi na hata mashabiki wamelitaja bao hilo kuwa ni la kuotea wakienda mbali zaidi na kusema kuwa ni kwa uhalisia sio bao halali na mwamuzi hakuwa makini. Maswali mengi yakielekezwa kwa waamuzi kutokana na namna wanavyoamua mechi za ligi, huku wengine wakifika mbali na kuhoji juu ya uwezo wao.

Naye kocha wa Yanga, Luc Eymael katika ukurasa wake wa Twitter ameweka video, akihoji jinsi bao hilo lilivyofungwa.

"Hii ndiyo namna Simba inashinda ubingwa?. Mara ya pili ndani ya wiki moja, tuwe wakweli jamani", amehoji kocha Eymael