Golikipa wa zamani wa Simba afariki mazoezini

Jumatatu , 13th Mei , 2019

Mchezaji wa timu ya Transit Camp ya Daraja la Kwanza Ahmad Waziri, amefariki ghafla  asubuhi ya leo baada ya kudondoka akiwa anatoka mazoezini na wenzake kwenye Kambi ya Twalipo, Kurasini Jijini Dar es Salaam. 

Ahmad Waziri alipokuwa akiitumikia Simba.

Kocha wa Transit Camp Nevi Kanza, ameeleza kuwa Ahmad, amefanya mazoezi ya leo asubuhi na wenzake  lakini wakiwa wanaelekea kupanda daladala maeneo ya Uhasibu aliteleza na kuangukia jiwe na alipokimbizwa hospitali alikuwa tayari aemshafariki.

''Tumefanya mazeozi vizuri lakini wakati tumemaliza tunaondoka pale uwanjani aliteleza akaangukia jiwe wakati ambao alikuwa kama anafunga kamba za viatu wenzake wakachukua usafiri wa bajaji na kumkimbiza hospitali na alipofika ikabainika kuwa tayari ameshafariki'', amesema Kenza.

Ahmad amewahi pia kuzichezea Simba SC, African Lyon, Majimaji FC, Mlale JKT na JKT Tanzania na kwa kipindi  hiki alikuwa akiitumikia Transit Camp ambayo inajiandaa kwaajili ya mechi za ‘play-off’, ili kujinusuru kushuka daraja kwenye ligi daraja la kwanza.