Jumatatu , 17th Jul , 2017

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemuachia huru Mkuu wa Kitengo cha Habari wa klabu ya Simba Haji Manara kuendelea na majukumu yake kama kawaida.

Hayo yameweka wazi na Mwenyekiti wa Kamati ya nidhamu Abasi Tarimba katika mkutano wake na waandishi wa habari mchana wa leo na kusema wamewafungulia baadhi ya viongozi waliowasilisha barua zao za kutaka kupitiwa tena upya hukumu zao.

“Wapo wengi waliofungiwa wengine maisha na wengine adhabu fupi, msamaha huu ni kwa wale ambao wameomba tu kupitiwa upya kwa adhabu zao, pia milango ipo wazi kwa wengine ambao wanataka kupitiwa kwa mashauri yao, lakini si kwa wale waliopanga matokeo uwanjani,” amesema Tarimba.

Pamoja na hayo, Tarimba amewaomba viongozi wa TFF kuandaa semina ya Maofisa Habari na Viongozi wa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ili kuepuka maneno machafu ambayo yanasababisha wao kufungiwa.

“Inaonekana viongozi na Maofisa Habari hawana maneno mazuri ya kuongea na wadau wa soka na ndio maana matatizo ya kufungiwa yanajitokeza mara kwa mara, naamini wakipata semina hiyo itawasaidia kujirekebisha na kupunguza kesi kama hizo,” amesisitiza Tarimba.

Manara alifungiwa na Shirikisho hilo Aprili 23, mwaka huu baada ya kubainika utovu wa nidhamu wa kutoa matamshi yasiyo na staha kwa viongozi wa TFF pamoja na vyombo vya uongozi wa mchezo huo na kupotosha umma dhidi ya kadi njano ya mchezaji Mohammed Fakhi wa Kagera Sugar ambapo alihukumiwa muda wa miezi 12 na kutakiwa kulipa faini ya shilingi milioni tisa adhabu iliyotolewa na Makamu  Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya TFF Wakili msomi Jerome.

 

 

.