Jumapili , 25th Apr , 2021

Rais wa shirikisho la soka Ulaya 'UEFA' Aleksander Ceferin amethibitisha vilabu vyote 12 vilivyotaka kushiriki mashindano mapya ya 'European Super League' vitaadhibiwa.

Rais wa shirikisho la soka Ulaya Aleksander Caferin

''Pamoja na mpango wao kutokufanikiwa, sisi kama shirikisho hatutakaa kimya tutawafundisha somo jipya kwa kuwaadhibu, ukiachilia mbali adhabu wanayoipata kutoka kwa mashabiki wao kwa maandamano na mabango kupinga jambo hili nasi hatutoacha kutoa yetu,'' alisema Ceferin.

Aliongeza, ''hatutataka kujua nani alikuwa kinara wa mpango huu, wala nani alikuwa wa kwanza kujiondoa katika jambo hili, hivyo tutashusha rungu kwa wote.''

Alipodadisiwa juu ya aina ya adhabu wanazotarajia kuzitoa alisema, ''hili litajadiliwa kwa kina japo kwa upande wa Uingereza huenda ikazidi kwa kuwa ilihusisha vurugu za mashabiki kupinga jambo hili japo nadhani haitaenda mbali na adhabu ya faini.''

Majuzi iliibuka taharuki kubwa sana juu ya kuanza kwa mashindano mapya ya ' European Super League' ambayo yalitafsiriwa yanakuja kukinzana na mashindano yaliyo chini ya UEFA kwa kuwa vilabu vyote vilivyotangaza kushiriki huwa vinacheza michuano hiyo.

Vilabu vya Manchester United, Manchester City, Arsenal, Chelsea, Liverpool na Tottenham kutoka Uingereza Juventus, Inter Milan na AC Milan kutoka Italy, Barcelona Atletico Madrid na Real Madrid kutoka Uhispania vilithibitisha kushiriki.