Alhamisi , 8th Apr , 2021

Mkurugenzi wa michezo nchini, Yusuph Singo ameiambia EATV kuwa, serikali imeadhimiria kushiriki katika mageuzi ya michezo kwa kujenga vituo mbali mbali vya michezo nchini ili kuibua na kukuza vipaji.

Mkurugenzi wa Michezo nchini, Yusuph Singo.

Singo amesema tayari Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imefanya mkutano kwa pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa 'TAMISEMI' na kukubaliana kufungua shule mbili za kukuzia vipaji kila mkoa.

“Mwaka huu tumeanza mkakati wa kufungua 'Center of sports excellence chuo cha maendeleo ya michezo Malya (Mwanza) kwa maana ya kwamba tutahifadhi vipaji, tutavitia vipaji, tutavitafuta vipaji, tutakuwa tunavikuza  pale kama serikali kutoa mfano ili kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo”.

Singo akasisitiza kuwa “Serikali imedhamiria, Serikali tayari imetenga fedha kidogo kwa ajili ya kuanzisha taifa cup ya vijana umri wa miaka 15 hadi 17 tutaianza mwaka huu Mungu akipenda”

Katika kufanikisha mageuzi hayo ya michezo nchini, Singo ametoa wito kwa wazazi kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha wana wasaidia watoto wao kujiunga kwenye vituo vya michezo.

“Wazazi watambue kwamba, Mungu ameumba binadamu na amewapa vipaji mbalimbali, wapo waliopewa vipaji vya kusoma, wapo waliopewa vipaji vyote na wapo waliopewa vipaji vya kufanya michezo, wazazi tuwaunge mkono watoto wetu kwenye vipaji ambavyo wanavyo”.

“Michezo sasa hivi ni ajira ina lipa pesa nyingi sana hakuna watu wanaolipwa pesa nyingi kama watu wa michezo. Kwahiyo wawe sehemu ya kuwanunga mkono watoto wetu ili wajiunge na vituo vya michezo ili waweze kuja kuwa wachezaji wazuri na kujipatia ajira”.