Jumapili , 5th Jun , 2016

Zoezi la usajili linandelea ndani ya Manchester United, baada ya timu hiyo kuweka mezani ofa ya kitita cha pauni milioni 30 kwa ajili ya kusaka saini beki kisiki wa Villarreal Eric Bailly na kuzipiku timu za Bayern Munich na Arsenal.

Beki wa timu ya Villarreal Eric Bailly wa mbele mwenye jezi ya njano

Kocha wa Manchester United Mreno Jose Mourinho anamatuamini ya timu yake kufikia makubaliano ya usajili wa beki wa kati Eric Bailly. Beki huyo kinda wa Villarreal mwenye umri wa miaka 22 amekuwa pia akitazamwa kwa ukaribu na vilabu mbalimbali barani Ulaya vikiwemo vya Manchester City, Bayern Munich na Arsenal lakini United sasa wameingia katika mbio hizo zakuwania saini ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani juu ya mazungumzo hayo dili la usajili wa beki huyo mpambanaji aliyejiunga Villareal mwaka 2014 kwa pauni milioni 4 akitokea Espanyol linataraji kuwa kiasi cha pauni milioni 18 pamoja na bonasi ya pauni milioni 12 na klabu hizo mbili zinamatumaini ya kufikia makubaliano haraka kwa ajili ya usajili wa beki huyo wa shughuli na mwenye ufundi na mbini nyingi uwanjani.

Beki huyo mwenye umbo lililojengeka kisoka Bailly jana hakuwepo kwenye kikosi cha Ivory Coast kilichocheza na Gabon huku pia mwanzoni mwa msimu huu mwezi Januari alihusishwa pia na maskauti wa vilabu vya Barcelona na Leicester ambavyo vimekuwa vikimfuatilia kwa muda mrefu lakini Villarreal wanaamini dili hiyo itafanikiwa kwa United.

Usajili wa beki huyo ni kama safari ya kocha Mourinho kuanza kutibu gonjwa la muda mrefu la United katika sehemu ya ulinzi hasa wa kati tangu kuondoka kwa walinzi mahiri wa kati kina Jaap Stam na Nemanja Vidic na nafasi hiyo ya ulinzi wa kati kuonekana kupwaya baada ya kina Daren Blind na Chris Smalling wakisaidiwa na kinda Thimothy Fosu-Mensa walioshindwa kuitendea haki nafasi hiyo.