Jumatano , 26th Jan , 2022

Michuano ya soka ya mataifa barani Afrika AFCON imetawaliwa na kadi nyekundu, na fainali za mwaka huu zimefunja rekodi ya kuwa na kadi nyingi zaidi ukilinganisha na fainali 4 zilizopita za michuano hii zimetolewa kadi 13 mpaka sasa, mashabiki walalamika.

Jumla ya kadi nyekundu 13 zimetolewa kwenye fainali za AFCON mpaka sasa zikiwa ni kadi nyingi ukilinganisha na fainali zilizopita

Kwenye muendelezo wa michuano ya AFCON hatua ya 16 bora jana ilichezwa michezo miwili na mfululizo wa wachezaji kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye fainali hizi za 33 za AFCON uliendelea baada ya kadi mbili nyekundu kutolewa kwenye mchezo kati ya timu ya taifa ya Senegal na Cape Verde. Ambapo kadi zote mbili walionyeshwa wachezaji wa Cape Verde kwenye mchezo huo ambao walipoteza kwa kunyukwa mabao 2-0.

Wachezaji wa Cape Verde waliopata kadi nyekundu kwenye mchezo huo ni kiungo Patrick Andrade na golikipa Vozinha na kufanya idadi ya kadi nyekundu kufikia 13 zilizotolewa mpaka sasa kwenye AFCON, zikwa ni kadi nyingi ukilinganisha na kadi zilizotolewa kwenye fainali 4 zilizopita ukizijumlisha kwa pamoja.

Kadi 7 kati ya hizo 13 zimetolewa kwenye hatua ya mtoano ya 16 bora ambapo ni mchezo mmoja tu ndio ambao haujashuhudia kadi nyekundu kati ya michezo 6 ya hatua hiyo iliyochezwa mpaka sasa, ni mchezo wa Morocco dhidi ya Malawi ndio mchezo pekee wa 16 bora ambao ulimalizika pasi kadi nyekundu kutolewa mchezo ambao Morocco imehinda kwa mabao 2-1.

Mchezo kati ya Burkina Faso na Gabon ilitolewa kadi nyekundu moja, sawa na kadi iliyotolewa kwenye Mchezo wa Nigeria na Tunisia na Cameroon na Comoro, kwenye mchezo wa Guinea na Gambia zilitoka kadi mbili nyekundu sawa na mchezo wa Senegal na Cape Verde.

Hatua ya 16 bora inakamilika leo kwa michezo 2, Je kadi nyekundu zitazidi kutolewa ama lah? Leo Ivory Coast wanacheza dhidi ya Misri Saa 1:00 Usiku na Mali wataminyana na Equatorio Guinea Saa 4:00 Usiku.

Na kumekuwa na malalamiko kwa mashabiki ambao wengi wao wameandika kupitia mtandao wa kijamii wa Tweeter wakipeleka lawama kwa waamuzi kuwa wanaaribu mashindano kwa kutoa kadi nyekundu hovyo baadhi yao wakilalamikia matumizi ya VAR kuwa ndio yanawapoteza waamuzi kwenye maamuzi wanayofanya.