Jumatatu , 20th Mei , 2019

Mshambuliaji wa klabu ya Simba, Meddie Kagere, anaongoza katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu akiwa na mabao 22.

Mshambuliaji, Meddie Kagere

Mchezaji huyo raia wa Rwanda, amefanikiwa kucheza kwa kiwango kikubwa msimu huu ikiwa ni msimu wake wa kwanza tangu alipojiunga kutokea klabu ya Gor Mahia ya Kenya, ambapo ameisaidia Simba kutoka nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hadi kuwa kinara hivi sasa ikihitaji pointi moja pekee kutawazwa bingwa.

Kwa idadi ya mabao aliyonayo hivi sasa, Meddie anahitaji mabao matatu zaidi ili aweze kuipiku rekodi ya mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu katika msimu mmoja, rekodi inayoshikiliwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, aliyefunga mabao 24 katika ligi mwaka 1994.

Magoli waliyofunga Kagere na wenzake

 

Yeye na washambuliaji wenzake Emmanuel Okwi na John Bocco kwa pamoja wamefunga jumla ya mabao 52 katika Ligi Kuu msimu huu, ikiwa ni zaidi ya mabao yaliyofungwa na klabu za Biashara United, Ruvu Shooting, Mwadui FC, JKT Tanzania, Kagera Sugar, Tanzania Prisons na Singida United.

Simba itapambana na Singida United, Jumanne, Mei 21 katika uwanja wa Namfua, huku ikiwa na uwezekano mkubwa wa kutangaza ubingwa katika mchezo endapo itapata pointi moja pekee na kufikisha jumla ya pointi 89 ambazo hazitofikiwa na klabu yoyote.