
Mohamed Hussein Zimbwe(Kushoto) na John Raphael Bocco(Kulia) wakisaini mkataba wa kuendelea kuitumikia Klabu ya Simba.
Tshabalala ambaye alikuwa akihusishwa na kutaka kuondoka kufuatia mkataba wake kubakisha muda mchache, alisaini jana sambamba na nahodha Mkuu wa kikosi hicho John Bocco.
''Kwa kifupi tupo pamoja, na ndio maana nimeongeza mkataba na timu yangu, kwasababu ni muajiriwa hapa kwahiyo napaswa muda wote kuitumikia, nafikiri hapa ni sehemu sahihi kwa maisha yangu ya mpira na maendeleo yangu hivyo naishukuru klabu yangu kwa kuniongezea mkataba''alisema Tshabalala.
Kwa upande wa nahodha mkuu wa klabu hiyo John Bocco ''Adebayor''amesema anaushukuru pia uongozi kwa kumpa nafasi ya kuendelea kusalia katika klabu hiyo.
''Naishukuru Klabu yangu kwa kuniamini na kunipa nafasi nyingine ya kuendelea kuitumikia, ni nafasi kubwa sana kwangu na ni nafasi ambayo kila mchezaji anaitamani katika karia yake ya mpira, kuanzia sasa mimi ni mchezaji wa Simba na nimeongeza mkataba, matarajio yangu ni kuendelea kuitumikia Simba kwa uadilifu ili kutimiza malengo ya klabu''alisema John Bocco baada ya kusaini mkataba mpya na Simba.
John Bocco alijiunga na Simba akitokea Azam msimu wa 2016/17 na kuwasaidia mabingwa hao watetezi kutwaa ubingwa kwa misimu yote aliyokuwepo msimbazi na hata kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili.
Naye Mohamed Hussein Tshabalala amedumu na kikosi hicho cha Simba kwa miaka saba mfululizo na kuitumikia kwa mafabnikio bila ya kuporomoka kiwango kwa muda mrefu.