Jumatano , 20th Jan , 2021

Kufuatia kipigo cha mabao 2-0 walichokipa timu ya taifa ya Tanzania Taifa stars kwenye michuano ya CHAN dhidi ya timu ya taifa ya Zambia, kocha mzoefu hapa nchini Meja mstaafu, Abdul Mingange ametupa lawama kwa makocha wa vilabu kushindwa kuwaanda wachezaji washindani

Taifa stars imepoteza mchezo wake wa kwanza wa kundi D kwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia

Baada ya stars kupoteza mchezo huo wa kundi D, Mingange ambaye amewahi kuvinoa vilabu vya Azam FC, Ndanda FC na sasa akiwa na kikosi cha Lipli ya Iringa ameiambia kipenga Xtra ya East africa radio

“Hata ukiangalia mchezaji mmoja mmoja wazambia walikuwa bora kuliko sisi na hii yote inatokana na sisi walimu kutofanya kazi huko kwenye vilabu wanakotoka wachezaji.Kuna makosa ya utumiaji wa miguu, kuna makosa ya upigaji wa pasi na makosa kwenye ile miondoko mitatu yani tukiwa hatuna mpira tunatakiwa twende wapi tukiwa na mpira twende wapi.Yaani uwezo wa mchezaji kujitambua wakati huu kuna jukumu gani, Hili sio jukumu la kumfundisha mtu timu ya taifa anatakiwa awe na misingi hiyo akiwa katika klabu yake”.

Licha ya kipigo hicho kwenye mchezo huo ambao ni wa kwanza kwenye hatua ya makundi lakini Taifa stars bado inamichezo miwili ya kujiuliza dhidi ya Namibia na Guinea,lakini Meja Mingange akaweka wazi juu ya kipi kocha Etienne Ndayiragije anapaswa kufanya ili kuhakikisha anapata ushindi kwenye michezo hiyo.

“Kwanza mwalimu abadilishe mbinu za mchezo, pili awaambie wachezaji wasifikirie matokeo yaliyopita, waanze na mechi inayokuja, akili yao itoke kwenye mechi iliyopita,kwasababu tumeshaipoteza hatuitaji kuihesabu.La tatu wachezaji wajue walichokikosea wasirudie tena, wafanyie mazoezi ili makosa tulioyaona hasa kwenye kukaba hasusani tunapokuwa hatuna mpira, nani anatakiwa awe wapi na kwa sababu gani, na ili ni tatizo kubwa sana kwa wachezaji wa Tanzania tena inatokana na uvivu”.

Taifa stars itatupa tena karata yake ya pili Januari 23 dhidi ya timu ya taifa ya Namibia, mchezo utakao chezwa Saa 4:00 Usiku.